Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameshtumiwa na mmoja wa wapinzani wake wakuu kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2017 kuhusiana na mbinu za uongozi wake.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

 Akiongea siku ya Jumapili, Evans Misati alisema kuwa gavana ameshindwa kukabiliana na visa vya ufisadi ambavyo vimekithiri kwenye serikali yake, huku akiongeza kusema kuwa gavana Nyagarama amekuwa akiwaajiri ndugu na marafiki kwenye serikali yake. 

"Sasa ni wazi kuwa gavana Nyagarama ameshindwa kabisa kuthibiti visa vya ufisadi kwenye serikali yake kwa kuwa hivi maajuzi tulisikia kuwa kulikuwa na lango la hospitali lililojengwa kwa kima cha shillingi milioni saba, na pia visa vya ufisadi vinavyowahusisha maafisa wake, na kwa sababu hiyo wananchi wamepoteza imani naye," alisema Misati. 

Misati aidha alimshtumu Nyagarama kwa kutowafuta kazi maafisa wanaohusishwa na visa vya ufisadi, huku na pia akiwahusisha wawakilishi wa wadi kwa kusitiri visa vya ufisadi vinavyoikumba serikali yake Nyagarama. 

"Gavana Nyagarama hajajitolea kukabiliana na ufisadi kwenye serikali yake, na ni jambo la kushangaza kwamba hata anashirikiana na wawakilishi wa wadi ili kuficha ukweli wa mambo kwa kuwa watu walionufaika na nafasi za ngazi ya juu za kazi ni jamaa na ndugu wa karibu," aliongezea.

Misati vilevile alimwomba gavana Nyagarama kutogombea ugavana kwenye uchaguzi mkuu ujao, na badala yake amuunge mkono mmoja wa wagombezi ili kujiepusha na aibu.