Vijana wa vikundi vitatu na wanaopata mtaji wao wa kila siku kwa kufanya biashara ya kuosha magari kwenye eneo bunge la Kitutu Masaba wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya mwanasiasa mmoja wa eneo hilo kuwanunulia pumpu tatu za kisasa za kuosha magari. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea katika shule ya msingi ya Gesibei, mwanasiasa huyo, Dkt Nyandoro Kambi aliwahimiza vijana kutotegemea kuajiriwa, na badala yake watafute namna ya kuanzisha miradi itakayowasaidia kujiendeleza. 

"Ninapoona vijana wamebuni kitu fulani kinachoweza kuwasaidia huwa nafurahi sana, na wakati sasa umefika kwa vijana kutafuta mbinu za kuanzisha miradi itakayowainua kimaisha badala ya kutegea kuajiriwa kwenye maofisi," alisema Kambi. 

Aidha aliwahimiza vijana hao kufungua akaunti za benki na kuweka faida zao kwenye akaunti hizo ili ziwawezeshe kupanua biashara zao, hali itakayowawezesha kuajiri watu zaidi. 

"Nyinyi vijana mnastahili kufungua akaunti za benki na kuhifadhi faida ya biashara yenu pale, na nina hakika kuwa biashara zenu zitakapopanuka, pesa hizo zitawasaidia kuajiri watu wengine zaidi, na kwa hivyo mtakuwa mmebuni nafasi za kazi kwa watu wengine kutoka eneo hili," alihimiza Nyandoro. 

Nyandoro alikuwa akihutubia makundi hayo ya vijana kutoka Manga, Nyansiongo na Chepilat kama njia moja wapo ya kuwapa motisha ya kujiendeleza maishani.