Hofu imetanda katika eneo la Ndimu Nakuru kaskazini baada ya mzee mmoja mwenye umri wa miaka 63 kupatikana ameuawa ndani ya chumba chake cha kulala usiku wa kuamkia Jumapili.
Akidhibitisha kisa hicho chifu wa kata hiyo Joseph Macharia alisema nyumba alimokuwa mzee huyo kulipatika shoka ambalo linadaiwa kutumika kutekeleza mauaji hayo ya kinyama.
"Tumeweza kupata shoka iliyotumika kumkata mwendazake, na tunashuku kuwa waliotekeleza mauaji haya ya kihayawani, walikuwa na lengo fiche," Macharia alisema.
Aidha chifu huyo alisema mkewe marehemu amedokeza kwamba, wakati wa mauaji yalitendeka alikuwa jikoni akiandaa cha kula cha jioni ambapo majambazi waliingia na kutekeleza kisa hicho.