Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani amekua mbunge wa kwanza aliyeasi muungano wa Cord kuadhibiwa na mrengo huo, baada ya jina lake kuondolewa katika kamati ya masuala ya bunge siku ya Jumanne.
Katika barua kwa bunge la taifa siku ya Jumanne, Cord ilieleza kuliondoa jina la Mwashetani katika kamati inayowaleta pamoja wanachama 29 kutoka mirengo ya upinzani na serikali, huku nafasi yake ikipewa mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Mombasa, Mishi Mboko.
Wiki iliyopita, mrengo wa Cord ulitishia kuwachukulia hatua wabunge waasi wa mrengu huo kwa kile walichokitaja kama kusalitiwa na wabunge hao, kutokana na hatua yao ya kufanya kazi na chama kipya cha JAP.
Tayari Cord imewaandikia barua wabunge hao huku ikiwataka kutoa sababu inayowafanya wasichukuliwe hatua kwa kufanya kazi na muungano wa Jubilee, licha ya kuwa walichaguliwa kwa vyeti vya Cord.
Kando na Mwashetani, wabunge wengine ambao huenda wakichakuliwa hatua na Cord ni pamoja na mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro, Peter Shehe wa Ganze, Salim Mustafa wa Kilifi Kusini na James Kamoti wa Rabai.