Mwekahazina wa kitaifa wa chama cha Kanu Dkt Elneo Nyakiba amemwomba kingozi wa mashtaka kwenye mahakama ya jinai huko ICC Fatuo Bensuoda kutupilia mbali kesi inayomkabili Naibu Rais William Ruto na Mtangazaji Joshua Sang kwa kuwa tayari wakenya waluokuwa wamehasiana wameweka tofauti zao kando na kutangamana. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kanisa la ADCG kule Kebirigo kaunti ya Nyamira siku ya Jumapili, Nyakiba alisema kuwa wakati umefika kwa kiongozi huyo wa mashtaka kutupilia mbali kesi hizo kwa kuwa amani imerejea nchini. 

"Inafaa Bensuada ajue kuwa tayari wale wakenya waliokuwa wamehasiana tayari wameweka tofauti zao kando na kukumbatia amani, na hiyo ni ishara tosha kuwa hamna chuki baina ya wakenya," alisema Nyakiba. 

Mwanasiasa huyo aliongeza kwa kusema kuwa linalostahili kufanywa na serikali ya Jubilee ni kuhakikisha kuwa wale watu waliofukuzwa makwao wamepata shamba za kuendesha shughuli zao ili warejelee maisha yao ya kawaida. 

"Linalostahili kufanywa kwa sasa ni kwa serikali kuhakikisha kuwa wale wakenya waliofukuzwa makwao wanapata pesa za kununua mashamba ili warejelee maisha yao ya kawaida," aliongeza Nyakiba. 

Nyakiba aidha alichukua nafasi hiyo kuwasuta wanasiasa wanaofanya misururu ya mikutano ya kuwaomboea Ruto na Sang akisema kuwa wanafaa kutekeleza miradi ya maendeleo. 

"Hatutaki kuona wanasiasa wakitumia pesa za umma kuzurura na kufanya mikutano ya kuwaombea naibu rais William Ruto na mtangazaji Joshua Sang, wanalostahili kufanya ni kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kutumia pesa za umma kufanya maombi yasiyo na msingi," aliongeza Nyakiba.