Mwekahazina wa kitaifa wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut John Matiang'i amesuta hatua ya tume ya mtihani Knec kufutilia mbali matokeo ya zaidi ya wanafunzi elfu mbili kote nchini waliofanya mtihani wa darasa la nane mwaka jana.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Ijumaa, Matiang'i alisema ni hatia kwa tume hiyo kufutilia mbali matokeo hayo ilhali chama cha Knut kiliposema mtihani huo ulikumbwa na visa vingi vya wizi tume hiyo ilikuwa kwenye mstari wa mbele kusuta madai hayo.
"Wakati visa vya wizi wa mtihani vilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari, chama cha Knut kiliitaka tume ya mtihani kufutilia mbali mtihani huo ila tume hiyo ikayasuta madai yetu vikali na sasa tunashangazwa na ni kwanini tume hiyo inafutilia mbali matokeo ya wanafunzi zaidi ya elfu mbili," alinena Matiang'i.
Matiang'i aidha alimtaka waziri wa elimu nchini Fred Matiang'i kuhakikisha matokeo ya wanafunzi athirika yametolewa, huku akiwahimiza walimu kutokubali kutia sahihi kandarasi ya utendakazi wao akihoji hiyo ni mbinu ya serikali kutaka kuwahujumu walimu.
"Waziri wa elimu sharti ahakikishe matokeo ya wanafunzi yaliyofutiliwa mbali yanatolewa, kwa maana hatujui sababu ya matokeo hayo kufutiliwa mbali hata baada ya Knec kukana kutokuwepo visa vya wizi wa mitihani na ni himizo langu kwa walimu kote nchini kutokubali kutia sahihi kandarasi ya ufanyakazi kwa maana tunaona kuwa hiyo ni njia mojawapo ya serikali kutaka kuwahujumu walimu," slihimiza Matiang'i.