Kiongozi wa muungano wa matatu katika Kaunti ya Mombasa Mburak Salim amepinga sheria za halmashauri ya uchukuzi na usalama nchini, NTSA akisema kuwa inaenda kinyume na ruwaza ya serikali ya Jubilee ya kuwatengea vijana kazi nchini.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa ni kinyume na matarajio ya wengi kuwa badala ya serikali kuwapa kazi vijana inawanyima kazi hasa katika sekta ya kusanifu michoro kwenye magari, na kuitaka halmashauri hiyo kuyaangalia vizuri masharti hayo na kuweka utaratibu ambao unaendana na mahitaji ya wahusika kwenye tasnia hiyo ya uchukuzi.
Mbarak amemtaka mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lee Kinyanjui kutafuta mwafaka kwa kuwahusisha washika dau wote kwenye uchukuzi ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anaridhika kufuatia hatua hiyo ambayo haijawafurahisha wengi.
Mwenyekiti huyo aidha amewahakikishia washikadau wote na wanachama wa eneo la Pwani kuwa watajitahidi kadri ya uwezo wao kuleta suluhu la kudumu kuhusiana na sheriia hizo.
Utaratibu huo ambao ulihusisha msako mkali dhidi ya magari ya abiria ambayo yanapaka rangi na michoro kinyume na sheria uliweza kuwaweka matatani wenyeji katika Kaunti ya Mombasa, huku wengi wao wakihiari kutembea kwa miguu kwa sababu ya kupandishwa kwa nauli, hali ambayo abiria hao walishtumu vikali na kuitaka serikali kuweka mwafaka na sheria kuzuia vitendo kama hivyo.