Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa Mamlaka ya umeme mashinani REA Simon Gicharu, ambaye pia ni mshikadau, mwanzilishi na mwenyekiti wa bodi ya Chuo Kikuu cha Mt Kenya (MKU), ameshtumu wizi wa mtihani ambao ulidhihirika katika mtihani wa KCSE mwaka jana.

Gicharu alisema kuwa ni muhimu chanzo cha wizi wa mitihani kubainika mapema na wala sio baada ya matokeo hayo kutangazwa.

Akizungumza mjini Nakuru siku ya Ijumaa, Bw Gicharu alitaka pande zote zinazohusika na maswala ya elimu, kushirikiana ili kumaliza udanganyifu huo katika kizazi kijacho.

“Wanafunzi wengi wanaendelea kuathirika na wizi wa mitihani ya kitaifa na ikiwa suluhu la haraka halitapatikana, basi huenda mustakabali wa watoto wengi ukaathirika pakubwa,” Alisema Bw Gicharu.

Hata hivyo, alipongeza Waziri wa Elimu Fred Matiang’i kwa kazi njema aliyosema anaendeleza katika wizara hiyo, kwa kuwa inaweza kuimarisha kiwango cha elimu nchini.

“Ningependa pia kumpongeza Waziri Matiang’i maanake juhudi anazodhihirisha katika kusuluhisha matatizo mbali mbali katika shule nyingi zinazaa matunda,” aliongeza Gicharu.

Gicharu pia alisema kuwa mamlaka ya REA itashirikiana na Wizara ya maji kuhakikisha shule zote ambazo zimepata nguvu za umeme pia zinapata maji safi ya kunywa na ya matumizi, ili kuimarisha viwango cha masomo.