Mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya ardhi Dkt Mohammed Swazuri amesema kwamba uamuzi wa mahakama wa kuikabidhi wizara ya ardhi majukumu ya kutoa hati miliki za ardhi ulilenga kutatua mvutano wa kimajukumu kati ya tume hiyo na wizara ya ardhi nchini.
Kulingana na Swazuri, tume hiyo iko tayari kushirikiana na wizara ya ardhi katika juhudi za kuhakikisha kwamba Wakenya kote nchini wanapata haki katika umiliki wa ardhi zao na wala sio kwa tume hiyo na wizara ya ardhi kuvutana kila uchao.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na tume hiyo, Swazuri amesema kwamba jukumu kubwa la tume hiyo kwa sasa ni kusajili ardhi zote na kuhakikisha kwamba swala la uskwota linadhibitiwa kikamilifu, huku akihoji kwamba taifa, hasa eneo la Pwani linakumbwa na migogoro mingi mno ya ardhi kwa sasa.
Hata hivyo, Swazuri ameitaka wizara hiyo ya ardhi kuyawajibikia majukumu yake kikamilifu ili kuona kwamba mizozo mingi ya ardhi nchini inakomeshwa na kila Mkenya anamiliki ardhi yake.
Kauli ya Swazuri inajiri siku chache tu baada ya mahakama ya juu zaidi kuamua kwamba jukumu la utoaji wa hati miliki za ardhi limo mikononi mwa Wizara ya ardhi nchini, huku tume hiyo ikipewa jukumu la kusajili ardhi zote nchini baada ya tume na wizara hiyo kufika mahakamani wakitaka ufafanuzi wa kimajukumu kati ya wizara ya ardhi na tume ya kitaifa ya ardhi.