Mwili wa msichana mwenye umri wa miaka 11 ulipatikana kwenye mto Darugu karibu na daraja la kuelekea Jordan, eneo la Bondeni mjini Nakuru.
Msichana huyo alikuwa ameripotiwa kupotea siku ya Jumanne wiki jana, hadi mwili wake ulipopatikana jioni ya Ijumaa mtoni humo.
Mkazi kwa jina John Kamau kutoka eneo hilo, ambaye aligundua mwili wa msichana huyo aliambia mwanahabari huyu kwamba alienda kuoga miguu kando ya mto huo ndipo alipogundua mwili wa msichan huyo baada ya kuona mwili wake unaelea.
Polisi wa kituo cha Bondeni waliitwa na kuuchukua mwili huo na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali kuu ya mkoa wa Nakuru- PGH, ukisubiri kufanyiwa upasuaji.
Akidhibitisha kisa hicho, OCPD wa Nakuru mjini Fred Lai alisema kwamba watatoa habari kuhusu kilichomuua marehemu baada ya upausaji huo, na kutupilia mbali dhana ya wakazi kwamba huenda mtoto huyo alinajisiwa na kisha kuuawa.
Visa vya unajisi na dhulma dhidi ya watoto wa kike haswa katika maeneo ya Gilgil, Njoro na Bahati vimeripotiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni.