Mwanamke mwenye umri wa makamu hii leo, Jumatatu alipatikana akiwa ameuwawa kwenye mtaa wa Umoja One, ulio Bahati viungani mwa mji wa Nakuru.
Mwili wa mwanamke huyo uliopatikana ukiwa uchi huku ukiwa na majeraha ulipatikana na wapitanjia mapema hii leo, Jumatatu, kabla ya maafisa wa polisi kujuzwa kuhusiana na tukio hilo.
Inaarifiwa kuwa marehemu, ambaye ni mama wa mtoto mmoja anadaiwa kuwa na matatizo ya kiakili, huku wakazi wa eneo hilo wakisema kuwa mama huyo alionekana mwisho Jumapili tarehe 13 Desemba.
Nguo zake zilipatikana mita chache kutoka kwa mwili wake ambao ulikuwa kwenye lindi la damu.
Mumewe marehemu alisema mke wake aliondoka nyumbani Jumapili mwendo wa saa moja asubuhi, lakini kufikia jioni hakuwa amerejea nyumbani.
Aliwajuza wanahabari kwamba alijaribu kumtafuta lakini hakumpata popote, akiongeza kwamba alimtafuta hadi kwenye eneo lililo karibu la Kubugia pombe haramu aina ya chang’aa ambapo alidaiwa kuonekanba lakini hakumpata.
Aliongeza kwamba ingawa mkewe huwa habugii vileo, huwa anatembelea eneo hilo la chang’aa mara nyingi ambapo yeye hutangamana na watu.
Maafisa wa polisi kutoka Lanet pamoja na wale wa makao makuu ya Githiori walifika katika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa mrehemu, ambapo waliupeleka katika hospitali wa kaunti ya Nakuru huku uchunguzi wa kubaini kilichosababisha kifo chake ukiendelezwa.