Wakazi wa mtaa wa Free Area viungani mwa mji wa Nakuru walisalia vinywa wazi siku ya Alhamisi baada ya kuupata mwili wa mzee mwenye umri wa maika 84 ukiwa unaoza ndani ya nyumba yake.
Mwili wa marehemu, Peter Njeru, uligunduliwa baada ya mke wa marehemu kumuita jirani yake, Mary Osindo, akimwarifu kwamba mume wake aliaga dunia siku ya Jumatano.
Hata hivyo, Bi Osindo alisema kuwa aligundua kwamba mwili wa mzee huyo ulikuwa umeanza kuoza huku upande mmoja wa uso wake ukiwa umeliwa na kile kinachoaminika kuwa panya.
Licha ya yaho, Bi Osindo alisema kuwa mkewe marehemu, Virginia Wanjiru, ambaye amekuwa akiishi kwenye nyumba hiyo tangu mume wake alipoaga, alisisitiza kwamba mzee huyo alifariki siku ya Jumatano.
“Bi Wanjiru aliniita na kuniambia kuwa mumewe ameaga dunia. Nilifika kwake haraka na kumpata akiwa ameketi na nilipomuuliza mwili wa mumewe ulipokuwa, aliniambia ulikuwa ndani ya nyumba. Nilipoingia ndani ya chumba chake, nilimpata mzee huyo akiwa amejikunja,” alisema Osindo.
Aliongeza: “Hapo niliamua kumuita Bi Wanjiru ili amweke mzee huyo vizuri. Alipomnyorosha mguu, kipande cha nyama kilianguka. Nilipomuuliza mzee huyo alifariki siku gani, alisisitiza kuwa mume wake aliaga dunia siku ya Jumatano.”
Ingawa marehemu alikuwa na ugonjwa wa mifupa wa 'arthritis', waliohojiwa na wanahabari walisema kuwa Wanjiru alikuwa akimwadhibu marehemu na wakati mwingine kumnyima chakula.
Chifu wa eneo hilo la Free Area, Stephen Kihara, alisema kuwa kutokana na hali ya mwili wa marehemu, haiwezekani kuwa alifariki siku ya Jumatano.
Kulingana na chifu huyo, marehemu mzee Njeru alikuwa na watoto wawili an alimuoa mke wake miaka 51 iliyopita katika Parokia ya Kanisa la PCEA Lanet.
“Nilipofika katika eneo hilo, nilipata maafisa wa polisi wa utawala wakiwa tayari wamewasili na nilipoingia ndani ya nyumba, nilipata mwili wa mzee huyo ukiwa kwenye chumba chake cha kulala. Baada ya kuingia pale na askari, tuliona mwili ule ni kama ambao ulikuwa umekaa pale kwa muda mrefu,” alisema Kihara.
Aliongeza: “Tulipiga ripoti kwenye Kituo cha polisi cha Mwariki na afisa mkuu wa kituo hicho akakuja na maafisa wake na kuuchukua mwili huo.”
Kwa sasa, mwili wa marehemu uko katika ufuo wa serikali ya kaunti ya Nakuru ukisubiri kufanyiwa uchunguzi kubaini chanzo cha kifo.