Polisi Machakos wamemtia mbaroni mzee wa umri wa miaka 50 eneo la Kiseini baada ya kumkatakata jamaa wa miaka 19.
Akidhibitisha kisa hicho, naibu chifu wa eneo hilo Samuel Nzale alisema kuwa wanaume hao walitofautiana na kumfanya mshukiwa kumshambulia mwathiriwa.
Walioshuhudia kisa hicho cha Jumapili mchana walisema wawili hao walikuwa kwenye mazungumzo wakati ambapo mzee huyo, ghafla, alikimbilia panga na kumkatakata jamaa huyo kichwani na kwenye mabega na kumwacha katika hali mahututi.
Nzale aliwataka wakaazi wawe wakitatua tofauti zao kupitia njia ambazo zinakubalika kisheria.
"Ni kisa cha kusikitisha kuona mzee anayepaswa kuwaongoza vijana wadogo ndiye anazua vurugu na kuleta madhara," Nzale alisema.
Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Machakos akisubiri kufikishwa mahakamani huku mwanamume aliyeumizwa aikpata matibabu katika hospitali ya Machakos Level 5.