Hali ya wasi wasi inaendelea kutanda katika eneo la Kosovo huko Ndabibi mjini Naivasha baada ya mzozo wa jamii mbili ambao umepelekea mtu mmoja kuaga dunia huku nyumba zikiteketezwa.
Ghasia hizo za jamii ya Wamaasai na Wakalenjin unahusiana na usimamizi wa shamba la ADC huku maafisaa wengi wa polisi wakitumwa eneo hilo.
Eneo hilo linapakana na kijiji cha Maella ambacho wiki jana kilikumbwa na mzozo wa umiliki wa ardhi ambapo mali ya dhamani kubwa yaliharibiwa.
Katika kisa cha mapema Jumapili eneo la Kosovo, jamii hizo zilianza mzozo wa umiliki wa ardhi hiyo ambao imekuwa ikizozaniwa kwa miaka mingi sasa.
Kiongozi mmoja aliyetambulika kama Josiah Sadera alisema kuwa mzozo huo ulianza Jumamosi jioni na kuendelea hadi Jumapili, huku kila upande ukidai umiliki wa ardhi hiyo.
“Ghasia hizi zilianza jana jioni hadi leo asubuhi na wanapigania ardhi hii ya shamba la ADC,” Alisema Sadera.
Kulingana naye, watu watatu wameachwa na majeraha ya mikuki huku mmoja wao anayeaminika kuwa hali mbaya akikimbizwa kwenye hospitali kuu ya wilaya ya Naivasha.
Mkuu wa tarafa ya Kongoni eneo hilo John Opondo amedhibitisha hali hiyo na kusema kuwa polisi tayari wamefika ili kurejesha hali ya usalama.