Baadhi ya wakazi wa Keroka wamemshtumu vikali gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama kwa jinsi anavyoshughulikia suala la mzozo wa mpaka wa Keroka baina ya serikali ya kaunti hiyo na Kisii.
Wakihutubia wanahabari kule Keroka siku ya Jumapili, wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na John Omanga walimtaka gavana kuichukulia hatua za kisheria serikali ya kaunti ya Kisii kwa kuendelea kutoza ushuru kwenye himaya ya kaunti ya Nyamira.
“Hili swala la mzozo wa mpaka baina ya kaunti ya Kisii na Nyamira ni suala lililosuluhishwa na viongozi wa kisiasa hapo awali, na inashangaza ni kwa nini serikali ya kaunti ya Kisii ingali inaendelea kutoza ushuru katika eneo hili,” alisema Omanga.
Wakazi hao aidha walisema kwamba wako tayari kuchukua hatua ya kuhakikisha kuwa eneo hilo la mzozo linasalia kuwa katika himaya ya kaunti ya Nyamira, huku wakiongezea kuwa hata sajili za mipaka zinaonyesha wazi kuwa eneo hilo la Keroka lipo Nyamira.
“Masoroveya walikuja wakapima eneo hili na kuamua kwamba lipo kwenye himaya ya kaunti ya Nyamira, na kwa maana kaunti hizi mbili ni za jamii ya Abagusii, ikaamuliwa kwamba kaunti ya Kisii imiliki sehemu ndogo ya eneo hili lakini ingali bado inatoza kodi kwenye himaya yetu na ndio maana sisi kama wakazi tumeamua kumsaidia gavana Nyagarama kuwaondoa watu hawa eneo hili,” aliongezea Omanga.