Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Shirika la kukabiliana na mihadarati na pombe nchini limeelekea mahakamani likitaka mahakama itoe agizo la kufungwa kwa baa zilizo katika eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru zilizowaruhusu vijana watano walioaga dunia kwenye ajali ya barabarani kubugia vileo.

Thibitisho hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Nacada John Mututho siku ya Jumanne, alipokuwa akizungumza katika eneo la Kikapu mjini Njoro kwenye ibaada ya mazishi ya mmoja wa vijana tano walioaga dunia mkesha wa kuamkia mwaka mpya kwenye ajali ya barabarani.

Mututho aidha aliashiria kwamba endapo madereva waliokuwa wakiendesha magari watazingatia sheria za trafiki, visa vya ajali vitapungua kwa kiasi kikubwa. 

Mututho amekariri kwamba shirika la Nacada litaendelea kupambana na utumizi wa mihadarati, huku akisisitiza kwamba mmliki wa baa hiyo iliyo katika eneo la Njoro iliyowauzia watoto hao pombe atajipata taabani hivi karibuni kwa kitendo hicho.

Ameonya kwamba mmliki huyo atalazimika kulipa fidia, huku akiongeza kwamba afisa wa polisi wa utawala aliyewapa watoto walioaga kwenye ajali hiyo gari lake pia huenda akajipata taabani.

Wakati huo huo, Mututho ameweka bayana kwamba hataki kiti cha ugavana kwenye Kaunti ya Nakuru kwa sasa, huku akimtaka Gavana Kinuthia Mbugua kushughulikia barabara ya Salgaa ili malori yaweze kuegeshwa.

Amekariri kwamba iwapo Gavana Mbugua hatachukua hatua hiyo kufikia wiki ijayo, atafanya harambee ili barabara hiyo iweze kutengezwa.

Izingatiwe kuwa vijana hao watano waliaga dunia kwenye eneo la Salgaa mkesha wa kuamkia mwaka mpya, baada ya gari lao kugongana na basi katika eneo hilo hatari ambalo hushuhudia ajali mbaya za mara ka mara.