Kufuatia tangazo la tume inayosimamia kura nchini IEBC, kuhusu kuwapa wananchi kazi ya kuwa maafisa wa kuwasajili wapiga kura vijana wa eneo la Nyamakoroto katika wadi ya Gesima wameombwa kutuma maombi ya kazi kwa wingi.
Akiongea katika baraza iliyofanyika mnamo Jumatatu 11, naibu wa chifu wa eneo la Nyamakoroto Paul Ombae amewaomba vijana kujitokeza kwa wingi.
"Hii ni nafasi murwa imetokea, na vijana wengi ambao hamna ajira nawaomba mjitokeze kwa wingi kwa kutuma maombi ya kazi na huenda wengi wenu wakapata nafasi," alisema Ombae.
Vile vile Ombae aliwahimiza walio wakongwe kujitokeza.
"Pia wakongwe hamjatengwa, jitokeze ili mpiganie nafasi hizi zilizo chache bora utimize yanayohitajika wakati wa kutuma maombi," aliongeza Ombae.
Usajili wa wapiga kura utachukua muda wa siku 30 kuanzia Februari 15 hadi Machi 15. Wanaotuma maombi ya kuwa maafisa wa usajili wanatarajiwa kumaliza mnamo Januari 15.
Uchaguzi mkuu utafanywa Agosti 8, 2017.