Wito umetolewa kwa wakaazi wa Kaunti ya Mombasa kushirikiana na maafisa wa polisi ili kuangamiza janga la dawa za kulevya.
Naibu kamishna wa polisi katika Kaunti ya Mombasa Salim Mahmoud amesema kuwa wananchi hawafai kuogopa kuwasiliana na polisi kwasabu usalama wao umeimarishwa.
Akiongea na mwandishi huyu katika ofisi yake, Mahmoud alisema kuwa swala la mihadarati limekuwa tishio kwa vijana wengi na kuwataka wakazi pamoja na wazazi kushirikiana ili kuhakikisha kuwa jinamizi hilo linatokomezwa.
Aidha, Mahmoud alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili katika kuwakamata walanguzi wa dawa ya kulevya ni kukosekana kwa ushaidi wa kutosha.
“Tuna changamoto katika kuwanasa walanguzi wa mihadarati kwa sababu wahusika si kama watumizi wa pombe. Wengine huweka dawa hizo za kulevya katika magari ya kubeba taka au majaa ya taka,” alisema naibu kamishna huyo.
Wakati huo huo, Mahoud alinyoosha kidole cha lawama kwa wananchi ambao wanawaficha walanguzi wa dawa za kulevya kwa kusema kuwa mitindo hiyo imelemaza kwa kiasi kikubwa juhudi zao za kupigana na ulanguzi wa mihadarati.
Eneo la Pwani hasa Kaunti ya Mombasa imekuwa na idadi kubwa ya vijana ambao wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya, jambo lillilomlazimu Rais Uhuru Kenyatta kutangaza pombe na dawa za kulevya kuwa janga la taifa.