Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wadi mteule katika Kaunti ya Nakuru amesema kuwa kuna upungufu wa walimu wanaotoa mafunzo ya dini ya Kiislamu ya 'Islamic Religious Education' (IRE), katika shule za Nakuru.

Akizungumza na mwandhisi huyu kwenye mahojiano siku ya Alhamisi mjini Nakuru, Ruth Cheptarus alisema upungufu huu umepelekea baadhi ya walimu wanaotoa mafunzo hayo shuleni kuchoka kwani wana madarasa mengi wanayofaa kufunza.

Alisema kuwa watawasilisha swala hilo kwa kadhi wa Nakuru ili liweze kutafutiwa suluhu la kudumu.

Kwa upande wake, Hawa Ibrahim Hassan, mwakilishi mteule katika Kaunti ya Nakuru, aliwahimiza wawakilishi wenzake kubuni sheria itakayoruhusu uwepo wa walimu wa dini mbalimbali shuleni, ili waweze kuwapa watoto wanoshiriki dini zao mafunzo ya kidini .

Wakati huo huo, aliangazia swala la baadhi ya wanafunzi wanaodhulumiwa shuleni kutokana na mavazi yao ya Kiislamu, kwa kusema hilo halifai kwani kulingana na katiba ya Kenya, kila mtu ana Uhuru wa kuabudu.

Cheptarus aliunga mkono usemi huo na kuwataka walimu katika shule mbalimbali kuwaruhusu wanafunzi wailsamu kuvalia mavazi hayo shuleni.

Pia aliwataka walimu hao kuwaruhusu wanafunzi hao kusali ifikapo wakati wao wa sala kwa muujibu wa dini hiyo.