Tume ya kitaifa ya uwiano na utangamano nchini NCIC imependekeza kushtakiwa kwa mwanasiasa ambaye pia ni mfanyiabisahara mjini Mombasa, Suleiman Shahbal, kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi.
Akizungumza mjini Malindi siku ya Ijumaa, katibu wa tume hiyo, Hassan Mohammed, alisema kuwa uchunguzi uliofanywa na maafisa wa NCIC umebaini kuwa matamshi aliyoyatoa Shahbal, mnamo Januari 2, 2016 ni ya uchochezi na yanaweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Mohammed vilevile aliwaonya wanasiasa wanaotoa matamshi yanayoweza kuleta mgawanyiko nchini, hususan wakati huu ambapo taifa linaelekea kwa uchaguzi wa 2017, kuwa watakabiliwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Mohammed alisema kuwa tume hiyo inapata changamoto katika juhudi zake za kupambana na wanasiasa kama hao, kwa kuwa haina uwezo wa kuwatia nguvuni, kwani hilo ni jukumu la maafisa wa polisi.
Shahbal alinukuliwa mapema mwezi Januari akisema kuwa mrengo wa Jubilee utashinda uchaguzi ujao “kwa ulazima hata kama ni kwa kuiba na kununua kura’’ katika mkutano wa kisiasa uliohudhuriwa na Naibu Rais William Ruto.
Matamshi hayo yalikashifiwa vikali na viongozi mbambali nchini na kumpelekea mkurugenzi wa mashtaka ya umma Kiriako Tobiko kuiagiza tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC pamoja na tume ya uwiano na utangamano NCIC kuyachunguza matamshi hayo.