Kamati itakayohusisha wawakilishi kutoka pande zote mbili za Kisumu na Nandi iliundwa Jumatatu mjini Nakuru kwa lengo la kurejesha amani katika maeneo hayo.
Kamati hiyo ilihalalishwa rasmi na kujumuisha vyombo vya usalaama, vijana, viongozi wa makanisa na kina mama baada ya kikao cha siku mbili kilichoandaliwa na tume ya uwiano na utengamano wa kitaifa NCIC.
Kwa upande wake mwenyekiti wa NCIC Francis Ole Kaparo, ambaye aliongoza zoezi hilo, amevipongeza vitengo vya usalama katika maeneo yote mawili kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuthibiti wizi wa mifugo uliokuwa ukishuhudiwa katika maeneo hayo.
“Tumeweza kuwanasa washukiwa 22 baada ya kikao cha mapema Januari katika eneo la Muhoroni kilichonuiwa kuleta amani,” Alisema Kaparo.
“Tume yangu itasaidia katika kutoa msaada wowote utakaopelekea amani ya kudumu katika meneo yaliyoathirika na taifa hili kwa jumla,” aliongeza.
Hata hivyo, makamishna wa majimbo yote mawili Kangethe Thuku na John Elunasa walisema usalama utaimarishwa katika mpaka, unaohusisha maafisa wa usalama 52, mbali na kuwepo mbinu ya kuripoti visa vya uhalifu iliyopewa jina mulika uhalifu katika jimbo la Nandi.