Share news tips with us here at Hivisasa

Shirika la takwimu nchini (NCPD) limekosoa wanasaisa wenye mmazoea ya kuhimiza Wakenya kupzaa watoto wengi bila kutilia maanani sera kuhusu mpango wa uzazi nchini.

Mkurugenzi wa huduma za kiufundi katika shirika hilo George Kichamu alisema wanasiasa kama hao wanapotosha Wakenya.

Kichamu alisema matamshi ya wanasiasa kama hao yanaweka vizingiti katika mpango wa serikali wa kutaka Wakenya wawe na familia bora ambazo wanaweza kugharamia mahitaji yao.

“Tunawashauri Wakenya wasikubali kuhadaiwa na wanasiasa ambao wanajitakia makuu pasipo kujali changamoto za kuwa na watoto wengi ambao hawawezi wakamudu mahitaji yao ya kimsingi,” alisema Kichamu.

Kichamu alikumbusha wanasiasa hao kwamba uchumi wa Kenya hauwezi ukaimarika iwapo Wakenya watazaa watoto wengi ambao hawatapata huduma bora za kimsingi.

Wakati huo huo, NCPD imesifia idadi kubwa ya wanaume nchini ambao wameanza kukumbatia mbinu za kisasa za upangaji uzazi zinazolenga wanaume.

Kwa mujibu wa shirika hilo, hali hiyo itachangia pakubwa uboreshaji huduma kwa jamii hasa familia za mapato ya chini.

Hatua hiyo inaoana na sera ya NCPD inayolenga kuona kwamba Wakenya wana idadi ndogo ya watoto ili wapokee huduma bora katika Nyanja zote.