Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kusimamia masuala ya utalii nchini Kenya Muriithi Ndegwa amepongeza hatua za serikali kwa kushirikiana na mataifa mengine kuona kuwa visa vya uharamia katika bahari Hindi vinapunguzwa na kuweka mazingira bora ya utalii.

Bwana Ndegwa amesema kuwa harakati hizo zimeanza kuzalisha matunda, na ni dalili nzuri kwenye taifa la Kenya kwa masuala ya utalii na huenda utalii ukaimarika zaidi kwenye msimu huu wa mwisho wa mwaka.

Alisema kuwa visa vya maharamia kuvamia meli za kuingia kwenye bandari ya Kenya ilichangia kupungua kwa watalii wanaozuru nchini kwa kuhofia usalama wao, na hivyo basi kunyima nchi hii mapato kutoka katika sekta hiyo.

“Kupitia juhudi za serikal za kupigana na uharamia pamoja na magaidi ambao walikuwa wanateka meli nyara katika bahari Hindi, sasa watalii wako huru kuzuru hapa kwetu bila hofu yoyote, na tunapongeza serikali yetu na wadau wengine kwa harakati zao,” alisema Ndegwa.

Ndegwa amesema katika hafla ya kuwapokea watalii kutoka nchi mbalimbali za ulaya ambao waliwasili alfajiri ya siku ya Ijumaa katika bandari ya Mombasa.

Watalii hao kutoka nchi za Ushelisheli, Marekani pamoja nan nchi nyingine za ulaya mbali na nchi ya Kenya wanatarajiwa kuzuru nchi nyingine za afrika mashariki kama visiwa vya Zanzibar na nchi ya Tanzania.