Rais Uhuru Kenyatta amesifiwa kutokana na kufanyia baraza la mawaziri mabadiliko na kutimua mawaziri waliokuwa wamehusishwa na ufisadi.
Mwakilishi wa wadi ya Bahati katika bunge la Kaunti ya Nakuru Peter Nderitu amempongeza rais kwa kuchukua hatua hiyo aliyoitaja kama ya 'ujasiri' akisema itasaidia kuimarisha utendakazi wa serikali ya Jubilee kupigana na ufisadi na kuinua uchumi wa taifa.
Akizungumza nje ya makao ya bunge hilo siku ya Jumatatu, mbunge huyo alisema kutorudishwa afisini kwa mawaziri waliokuwa wamesimamishwa kazi kwa madai ya ufisadi ni ishara tosha kuwa rais amejitolea kulikabili jinamizi la ufisadi.
“Ninaamini kwamba kiongozi wa taifa ana nguvu na uwezo wa kukabiliana na ufisadi. Singetaka kusema kulikuwa na ubaguzi kama viongozi wengine wanavyosema, ninaamini kwamba wote walioteuliwa, waliteuliwa kufanyia wakenya kazi, si makabila yao,” alisema Nderitu, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama katika bunge hilo.
Wiki iliyopita, rais Uhuru alifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri ambapo Mwangi Kiunjuri kutoka Laikipia Mashariki alichukua nafasi ya Anne Waiguru, ambaye alijiondoa kwenye wizara ya ugatuzi kufuatia shinikizo kali zilizotokana na ufisadi kwenye wizara yake.