Mwakilishi wa wadi ya Bahati katika bunge la kaunti ya Nakuru, ameitaka hazina kuu kubuni mikakati ya kutoa kwa haraka bila ya kuchelewa, fedha zinazostahili kutumiwa na serikali za kaunti katika maendeleo.
Akiongea katika shule ya upili ya Ronens Bahati Jumanne, Peter Nderitu Mwangi alisema kwamba kuchelewa kutolewa kwa mgao wa fedha hizo kunaadhiri pakubwa utendakazi wa serikali za kaunti, akitoa mfano na pesa za kufadhili masomo ya wanafunzi wanaotoka familia maskini.
“Wazazi walijaza fomu za basari mwezi Juni,2015, lakini pesa zimepatikana januari,2016. Hii inatufanya kama wawakilishi wa wadi kuwa na kibarua kigumu kuelezea wazazi kwa nini hawajapata basari” akasema Nderitu.
Aliongeza kuwa mtaala mzima unaotumika na serikali za kaunti katika utoaji wa kandarasi unafaa kurekebishwa, ili kurahishisha utoaji wa fedha kwa minajili ya utekelezwaji wa maendeleo.
“Italazimu tufanye maendeleo kulingana na jinsi fedha zinavyotolewa kulingana na bajeti, kwa hivyo wale ambao hamjapata maji kama maeneo ya juu ya kata ya Kamiruri, tutafanya juhudi mwaka ujao wa kifedha kuwasilisha pendekezo la kujenga tenki la maji eneo hilo,” akasema huku akijibu swali kutoka kwa wakaazi.
Hata hivyo maeneo mengine kama Landimawe, wenyeji wanafurahia maji ya mifereji ambayo iliwekwa maajuzi.