Aliyekuwa katibu wa kudumu Richard Ethan Ndubai ameapishwa rasmi kama mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa vijana NYS.
Akizungumza kwenye sherehe ya kuapishwa kwa mkuregenzi huyo katika Ikulu ya Mombasa siku ya Jumanne, Rais Uhuru Kenyatta aliagiza kuanzishwa kwa mradi wa maendeleo kwa vijana.
Raisi alisema kuwa lengo kuu la kuboresha maisha ya vijana ni kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Rais Kenyatta alisema kuwa mradi huo utaanza katika kipindi cha miezi miwili ijayo.
“Ujuzi utakaopewa vijana hao kupitia mradi huo utaleta amani na uwiano nchini,” alisema Kenyatta.
Aidha, rais alisema kuwa kazi ya mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa vijana itakuwa ni kuwaondoa wale wanayoiangusha idara hiyo.
Hafla hiyo iliongozwa na mkuu wa watumishi wa umma Joseph Kinyua.