Mkurugenzi mpya wa shirika la kitaifa la huduma kwa vijana NYS Richard Ethan Ndubai anakabiliwa na kibarua cha kuhakikisha anasafisha shirika hilo dhidi ya ufisadi pamoja na kuwaondoa maafisa wote wanaoshukiwa kuhusika na ufisadi.
Siku ya Alhamisi, msemaji wa ikulu ya Rais Manoah Esipisu alisema Rais Uhuru Kenyatta analenga kuboresha maisha ya vijana humu nchini hivyo basi kuamrisha kuanza rasmi kwa mradi huo katika miezi miwili ijayo.
Akihutubia wanahabari katika ikulu ya Mombasa alisema kuwa mradi huo utaanza upya katika kaunti za Mombasa na Kilifi kwa kusafishwa kwa soko la Kongowea na mji wa Mtwapa.
Wakati uo huo amepuuzulia mbali taarifa zilizochapishwa katika baadhi ya magazeti humu nchini kuwa mkurugenzi huyo alikabidhiwa ardhi kinyume cha sheria miaka 20 iliyopita.
Esipisu alisema baada ya mkurugenzi huyo kutajwa katika ripoti ya Ndun’gu alikabidhi ardhi hiyo kwa serikali mwaka 2006 baada ya kutakiwa kufanya hivyo na tume ya kupambana na ufisadi ili kusafisha jina lake.