Mkurugenzi wa bodi ya shirika la kupambana na ulanguzi wa mihadarati na vileo nchini NACADA, Sheikh Juma Ngao ameitaka serikali kuiongezea fedha zaidi shirika hilo ili kudhibiti kuenea kwa ulanguzi wa mihadarati nchini.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Ngao amesema kuwa shirika hilo linakabiliwa na changamoto za kifedha, hivyo basi maafisa wa shirika hilo hushindwa hata kuzuru mashinani kuwaelimisha wakenya hususan wanafunzi dhidi ya kujikinga na utumizi wa mihadarati.
Sheikh Ngao amesema kuwa shilingi milioni 160 walizotengewa na serikali katika kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati nchini hazitoshi kufanikisha jukumu hilo, na akamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuitengea fedha zaidi shirika hilo.
"Fedha tulizotengewa na serikali kamwe hazitoshi kwa maafisa wetu kuzuru hata mashinani kuielimisha jamii dhidi ya kujiepusha na mihadarati, na iwapo serikali itasalia kimya na jambo hili, basi sioni tukikabiliana vyema na mihadarati nchini wala eneo hili la pwani," alisema Ngao.
Mkurugenzi huyo wa bodi aidha alisema amesikitishwa na tatizo la mihadarati nchini na hususan eneo la Pwani kuwa donda sugu licha ya baadhi ya viongozi na maafisa wa usalama kuwafahamu vyema walanguzi wakuu lakini hakuna hatua zozote dhidi yao zimechukuliwa.