Mbunge wa Bahati, kaunti ya Nakuru Onesmus Kimani Ngunjiri amewataka walimu katika eneo bunge lake kuwajibika vilivyo kuhakikisha kuna matokeo mema.
Akizungumza Alhamisi katika shule ya upili ya Heroes kwenye wadi ya Kabatini Ngunjiri amesema kuwa matokeo mema yataafikiwa tu iwapo walimu watapenda kazi yao kando na changamoto zilizopo.
"Najua kuna changamoto si haba katika sekta ya elimu lakini la muhimu ni walimu mpende kazi yenu na kuwajibika hata zaidi," alisema Ngunjiri.
Akiwahutubia walimu na wanafunzi katika shule hiyo, Ngunjiri amesema kuwa atazidi kuhakikisha kila mtoto eneo bunge hilo anapata elimu bora.
Amekariri kwamba elimu ndio nguzo muhimu ya taifa hili na haifai kuingizwa siasa.
Wakati uo huo amewataka walimu na wazazi kushirikiana kwa matokeo bora.