Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amewasuta maafisa wa polisi mjini Nakuru kwa kumkinga spika wa bunge la Kaunti ya Nakuru Susan Kihika katika mzozo uliopo kati yake na mwekezaji moja huko Bahati.
Akiongea na wanahabari mjini nakuru siku ya Jumapili, Ngunjiri alisema kuwa spika Kihika anapaswa kukamatwa kwa kuvamia mali ya mtu binafsi na kuiharibu, lakini polisi hawataki kumkamata.
"Kihika alituma watu kubeba mali ya mtu na hiyo mali ikapatikana kwa nyumba yake lakini polisi wamedinda kumkamata," alisema Ngunjiri.
"Polisi wa Nakuru na mkubwa wao hawataki kutenda haki na wanamwacha spika huyo kuwa huru," aliongeza.
Ngunjiri alikuwa akizungumzia swala ambapo spika Kihika anamshtumu kwa kuingilia maswala ya familia yao na kuchochea mzozo baina ya wajane wa marehemu Kimani Kihika.