Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amewataka viongozi kutoka kaunti ya Nakuru kukomesha siasa za malumbano na badala yake wawahamasishe wananchi kujiandaikisha kama wapiga kura.
Ngunjiri amesema kuwa inasikitisha kuona wanasiasa waking’ang’ana kutafuta kuchaguliwa ilhali raia hawajiandikishi kama wapiga kura.
Akiongea Jumatano katika eneo bunge lake la Bahati, Ngunjiri aliwaonya wanasiasa kuwa huenda wakakosa kuchaguliwa iwapo wanaowatarajia wawapigie kura hawatajiandikisha.
“Mimi nashangaa sana ninapoona watu wakiharibu wakati kupiga siasa lakini hawambii watu wajiandikishe kama wapiga kura.Badala la kupiga siasa tupu wacha tuanze kuzunguka tukiwatoa watu waende wajiandikishe kama wapiga kura,” alisema Ngunjiri.
Ngunjiri aliwataka wakaazi wa kaunti ya Nakuru kujiandikisha kwa wingi iwapo wanataka Rais Uhuru Kenyatta aendelee kusalia mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
“Uhuru hawezi endelea na kazi kama watu wa Nakuru hawatajiandikisha kama wapiga kura kwa sababu huwezi mpigia kura kama hujajiandikisha kama mpiga kura,” alisema.
Aliwataka wabunge wote wanaohudumu kwa sasa kutoka Nakuru kutumia muda wao mwingi katika kuwahamasisha raia kujiandikisha kama wapiga kura.