Kiongozi kamili ni asiyebagua wasiojiweza na walemavu, kutoka kwa wanaojiweza kimaisha, Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amesema.
Kimani akizungumza lJumatano na zaidi ya walemavu mia tano kutoka eneo bunge hilo, katika uwanja wa shule ya msingi ya Kiamaina, alielezea kuhuzunishwa kwake kutokana na ukosefu wa mikakati kwenye serikali ya kaunti ya Nakuru, itakayowaondoa walemavu kutoka kwenye kundi la kulipa kodi.
Kimani aliichangamoto serikali ya kaunti hii kukoma kutoza walemavu ushuru, akisema wengi wao ni ‘maskini wasio na pesa.’
Licha ya kwamba siku ya walemavu kote duniani husherehekewa tarehe 3 ya kila mwezi Disemba, mbunge huyo wa TNA aliamua kukusanya walemavu hao na kuwapa ‘sikukuu ya mapema’ kwa kuwagawia chakula ikiwemo unga na mchele.
“Kwa sababu kesho nitakuwa bungeni, leo nimeamua niwaletee sikukuu, na tuzungumze kuhusu mambo yanayowaadhiri kama walemavu” akasema Kimani.
“Ubaguzi dhidi ya walemavu hauna nafasi katika karne ya sasa, kwa hivyo ningependa kuona serikali ikiajiri walemavu zaidi kwenye makampuni na mashirika mengine hata ya kibinafsi” alisisitiza Kimani, huku akisema kwamba yeye binafsi amemweka mtu anayeishi na ulemavu katika ofisi yake ya CDF, kando na kushinikiza kampuni ya GDC kumwajiri mlemavu atakayewawakilisha wenzake kwenye kampuni hiyo.