Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, sasa anataka maafisa wote wa serikali waliotajwa na aliyekuwa waziri wa ugatuzi Anne Waiguru kwa madai ya kuhusika na ubadhirifu wa fedha katika shirika la NYS kujiuzulu mara moja.
Kimani Ngunjiri anasema kuwa maafisa hao “wanapaka tope utendakazi wa serikali ya Jubilee.”
Akizungumza kwenye runinga ya K24 Jumatano, Ngunjiri pia alitahadharisha wahusika wa sakata hiyo kutomhusisha naibu rais William Ruto katika sakata hiyo.
“Kutajwa kwa msaidizi wa naibu rais, si kumaanisha Ruto mwenyewe amehusika. Kwa hivyo nawaomba hawa wenzetu wa Cord wasiingize siasa zao kwa Ruto kama vile wamezoea,” alisema Kimani.
Kimani alisema hayo baada ya waziri wa zamani katika wizara ya ugatuzi Ann Waiguru, kupasua mbarika Jumanne na kumhusisha kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Adean Duale, naibu kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen na msaidizi wa naibu rais Farouk Kibet na sakata inayohusu kupotea kwa mamilioni ya fedha katika shirika la NYS.
Katika hati ya kiapo aliyowasilisha mahakamani Waiguru anamlaumu seneta Kipchumba Murkomen kwa masaibu yanayomkabili.
Kulingana na Waiguru, seneta huyo alimtishia kuwa endapo hatasitisha uchunguzi kuhusu milioni 791 za NYS zilizopotea atapanga njama ya kumpaka tope.