Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi wa eneo la Kinungi eneo bunge la Naivasha kaunti ya Nakuru, sasa wanataka viongozi wa kanisa kuandaa maombi ya kutakatifisha eneo hilo, kutokana na ongezeko la ajali zinazoshuhudiwa kila uchao.

Wakaazi hao walisema kwamba huenda eneo hilo linatumika kutoa kafara maisha ya binadamu, kwani haipiti siku mbili kama ajali haijatokea ambapo maafa hupatikana.

Hayo yanajiri baada ya mwanamme aliyekuwa akivuka barabara kugongwa na kuuawa na gari lililopotea usiku wa Jumapili, na baada ya mtu mwingine kugongwa na kuuawa na gari yapata kilomita moja kutoka hapo siku ya Jumamosi, kando na visa vingine viwili kwenye barabara ya Naivasha mai mahiu ambapo motto na mtu mzima pia walipoteza maisha.

Mkaazi Mary Gerald alisema serikali kuu na ya kaunti ya Nakuru, zimeendelea kupuuza kuweka matuta eneo hilo, licha ya maandamano kufanyika kila kunapotokea ajali. "Kwa sababu tumeililia serikali haisikii, pengine ibada ikifanywa hapa na makanisa yote, tunaweza ondoa mashetani ambayo huenda yamewekwa hapa" akasema mkaazi Mary.

Naye dereva Mwaura anayehudumu na gari la NAGIL kutoka Nakuru-Naivasha-FlyOver, alisema eneo hilo linahitaji maombi sasa.

“Japo kuna abiria ambao huvuka barabara bila kuangalia, na madereva ambao huendesha gari wakiwa walevi, ama kwa mwendo wa kasi, kama mtu ambaye ameokoka, siamini hizi ajali ni za kawaida, kwa hivyo tunahitaji maombi. Karibia kila boma la hapo Kinungi sasa lina mtu aliyekufa ama aliyeumizwa kupitia ajali.

Mkaazi mwingine Lucy Magode, alisema ingekuwa heri usimamizi wa barabara kuu nchini kuchunguza ni kwa nini magari huendeshwa kwa mwendo wa kasi kwenye barabara ya Nakuru Nairobi.

“Kuna uwezekano hao madereva husafirisha bidhaa haramu kama bunduki na pembe” akasema bi Lucy.

Jumapili usiku Polisi wa kupambana na ghasia walilazimika kufika eneo hilo na kuwatawanya umati wa wenyeji walioifunga barabara hiyo kwa zaidi ya saa nne kulalamikia ajali hiyo.

Na huku polisi wakidhibitisha ajali hiyo, OCPD wa Naivasha Titus Munyoki amesema kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari.