Kamishna mkuu wa shirika la ukusanyaji wa ushuru nchini KRA John Njiriani amesema hatua ya kufunga mashirika mawili ambayo yanahusishwa na gavana wa Mombasa ilifuata sheria.
Njiraini amesema kuwa shirika la KPA lilibaini kuwa kufungwa kwa mashirika hayo ni moja ya hatua za kisheria ambazo huchukuliwa ili kufanya uchunguzi kuhusiana na ukwepaji wa sheria za ushuru nchini.
Kwenye arifa zilizotumwa kwenye vyombo vya habari siku ya Jumamosi, kamishna huyo alisema shirika la kukusanya ushuru nchini KRA litaendelea kutumia sheria kama njia moja ya kuimarisha ukusanyaji wa kodi nchini, na kuwakabili baadhi ya watu binafsi na mashirika ambayo huenda yanaepa kulipa kodi.
“Shirika letu litawachukulia hatua za kisheria baadhi ya mashirika ya bandarini ambayo yanahusika kwenye biashara ambazo ni haramu,” alisema kwenye arifa hiyo.
Wafanyibiashara pamoja na wafanyikazi waliokuwa wakihudumu katika mashirika hayo, bado hawajajua hatima yao ni ipi ikizingatiwa kuwa bado hakuna hatua yoyote imechukuliwa kuhakikisha kuwa mashirika hayo yanafunguliwa, na kutoa mali yaliyo kwenye makasha ya wateja wa mashirika husika.
Shirika la KRA na lile la KPA bado limeshikilia msimamo mmoja hadi pale uchunguzi kuhusiana na mashirika hayo utakapokamilishwa.
Kufungwa kwa mashirika hayo tayari kumeleta joto kati ya viongozi wa Pwani na shirika la bandari nchini, huku viongozi hao wakiitaka KPA kuyafungua masharika hayo, na kutishia kuchukua hatua ambayo waliiweka fiche.