Share news tips with us here at Hivisasa

Huku ndege ya Ufaransa ikitua katika angatua ya Moi Mombasa mapema Jumapili, waziri wa masuala ya usalama wa ndani Joseph Nkaisserry amepongeza idara ya usalama katika Kaunti hiyo kwa kuchukua hatua za haraka na dharura ili kuhakikisha kuwa wasafiri ambao walikuwa wanaelekea jijini Paris wako salama.

Akongea jijini Mombasa baada ya kuzuru na kujionea ndege hiyo ambayo ilikuwa na zaidi ya abiria 455, waziri huyo alisema kuwa maafisa wa usalama katika jimbo hilo walilishughulikia swala hiyo kwa njia ya kitaalam, na kuwataka kuendelea na mchakato na moyo huo wakati wote.

Waziri Nkasserry aliwahakikishia wasafiri hao kuwa serikali ya Kenya itafanya kila linalowezekana ili kuona kuwa abiri wote waliokuwa katika ndege hiyo ya Air France wanasafirishwa kuelekea maeneo walikokuwa wanakwenda kwa kutumia njia mbadala.

“Ninawapa heko sana maafisa wa usalama wa Mombasa kwa kushughulikia swala hili kwa njia ya inayofaa na tunawahakikishia abiria waliokuwa katika ndege hii kuwa usalama wao unaangaliwa na wasiwe na shaka,” alisema Nkaiserry.

Hata hivyo, huenda ndege hiyo ikaendelea na safari yake hii leo, Jumatatu kulingana na afisa mmoja wa operesheni wa ndege baada ya uchunguzi kukamilika kutafuta bomu lililodaiwa kupachikwa katika kimojawapo cha choo cha abiria kulingana na habari zilizowasilishwa kwenye kitengo cha mawasiliano cha ndege hiyo na kusambaziwa vyombo vya habari vya kimataifa.