Serikali sasa imefutilia mbali uuzaji wa ardhi yenye ekari 3,000 kwa shirika la KenGen kutoka kwa kampuni ya kununua shamba ya Ng'ati mjini Naivasha.
Vile vile, serikali itaanzisha uchunguzi ili kujua jinsi ardhi hiyo ilivyouzwa tukio ambalo limepelekea mzozo wa wakulima huku nyumba na mali ya dhamani kubwa yakiharibiwa.
Haya yamejiri baada ya Waziri wa Usalama wa Kitaifa Joseph Nkaissery kuwaongoza maafisa wakuu serikalini Jumanne kwenye ziara ya eneo la Maella mjini humo ambalo limekumbwa na ghasia za wiki nne sasa.
Nkaisery amesema kuwa haieleweki jinsi ardhi hiyo iliuzwa kwa shilingi milioni 505 huku wakulima ambao ni wanachama wa shamba hilo wakipata shilingi milioni 294 pekee.
“Swala hili linahitaji uchunguzi wa kina na udharura kwa sababu haieleweki jinsi ardhi hii ilivyouzwa,” alisema Nkaissery.
Kutokana na hayo waziri huyo ameagiza pia kutiwa nguvuni kwa wakurugenzi watano wa Ng'ati waliohusika pakubwa kwenye uuzaji huo na kusema walifaa kurekodi taarifa kwa polisi.
Aidha ameagiza kuwa shule zilizofungwa zifunguliwe na wakulima waliotiwa mbatoni na kukosa bondi kuachiliwa kwa bondi ya bure.
Naye mbunge wa Kabete Ferdinand Waititu amedai kuwa kila mkuu wa wilaya na OCPD ambaye amewahi kuhudumu eneo la Naivasha walibahatika na ardhi hiyo, na kuongeza kuwa wanafaa kuchunguzwa.
Kwa upande wake MCA wa eneo hilo Kariuki Mujina amemtaka waziri huyo kuwaagiza polisi kukoma kuwahangaisha wakazi hao ambao wamekuwa wakilala kwenye msitu tangu ghasia hizo kujiri.