Halmashauri ya usafirishaji na usalama barabarani (NTSA) imesema kuwa itaimarisha misako katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret wakati wa likizo ya Krismasi.
Afisa mkuu mtendaji wa NTSA Francis Meja amesema kuwa misako hiyo itaimarishwa nyakati za mchana na usiku ili kuhakikisha kuwa madereva wanazingatia sheria za trafiki ili kupunguza maafa barabarani wakati wa krismasi.
Akiongea mjini Nakuru Alhamisi Meja alisema kuwa watashirikiana na maafisa wa trafiki katika doria hizo.
“Tunajua wakati wa krismasi ajali katika barabara kuu ay Nairobi –Eldoret huongezeka sana na kwa hivyo tutazidisha misako na doria katika barabara hiyo wakati wa usiku na mchana kwa nia ya kupunguza ajali zinazotokea na wizi wa barabarani,” alisema Meja.
“Misako hiyo itajumuisha maafisa wa NTSA na wale wa trafiki na tutawalenga madereva wanaovunja sheria za trafiki na pia wezi wanaowalenga watumizi wa barabara haswa nyakati za usiku,” akasema.
Meja alisema kuwa doria kali itawekwa katika maeneo ya misitu ambapo wizi mwingi an utekeja nyara wa magari hufanyika.
“Maeneo yalio na misitu kwenye barabara hii yatashuhudia doria kali maanake hapo ndipo utekaji nyara mwingi hufanyika na pia tunawataka madereva kuwa waangalifu wanapofika maeneo hayo ili kupunguza hatari ya kutekwa nyara na majambazi,” alisema Meja.