Halmshauri ya usafiri na usalama wa barabarani NTSA, pamoja na halmashauri ya kitaifa ya barabara kuu 'Kenya National Highways Authority' zimehimizwa kufanya kazi pamoja kwa minaajili ya kukabiliana na misongamano ya barabarani ambayo hushuhudiwa mara kwa mara katika eneo la kupimia uzani wa lori mjini Gilgil.
Himizo hilo lilitolewa na spika wa bunge la Kaunti ya Nakuru Susan Kihika aliyekuwa akizungumza alipotoa zawadi za krismasi kwa wakongwe mjini Gilgil siku ya Alhamisi.
Kihika alisema kuwa katika siku za hivi maajuzi, kumeshuhudiwa misongamano katika eneo hilo, hali ambayo inawatatiza wengi.
Spika Kihika alisema kuwa iwapo swala hilo halitashughulikiwa, huenda watu wengine wakakosa kuungana na familia zao kwa sherehe za krismamsi na mwaka mpya.
“Kucheleweshwa huko ni pigo katika ujenzi wa taifa ikizingatiwa kwamba muda mwingi unapotezwa huku wengi wakijarimu kujikwamua kutokana na misongamano hiyo,”alisema Kihika.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wadi ya Gilgil Jane Ngugi ambaye pia alihudhuria hafla hiyo, alisema ni jambo la kuudhi kuona kwamba licha ya viongozi kuangazia swala hilo na kujuza mamlaka husika, hakuna hatua ambayo imechukuliwa kufikia sasa.
Ngugi alisema kuwa hali hiyo huenda ikawa mbaya zaidi wakati wa sherehe za krismasi, kwani watu wengi husafiri kujumuika na familia zao wakati huo.
Zaidi ya watu mia moja walifaidi kutokana na msada huo uliotolewa na Spika Kihika.
Kihika pia alihimiza mashirika mbalimbali kujitokeza na kuungana mikono kuwasaidia wanaohitaji msaada katika Jamii.