Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa halmashauri ya usafiri an usalama barabarani Lee Kinyanjui amewashtumu wakenya wanaotumia barabara kwa kupuuzilia mbali umuhimu wa kufunga mikanda ya usalama wanaposafiri.

Kinyanjui amesema kuwa tabia ya wakenya kutofunga mikanda ya usalama inachangia pakubwa katika ongezeko la vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Akiongea Jumamosi wakati wa hafla moja ya harambee mjini Nakuru, Kinyanjui alisema kuwa utafiti umeonyesha watu wanaohusika katika ajali wakiwa wamefunga mikanda huepuka bila majeraha ama na majeraha madogo.

“Wakati unapofunga mkanda wa usalama unakuwa unajikinga wewe mwenyewe na kujiepusha na maafa iwapo ajali itatokea. Lakini wakenya tumezoea kusafiri vifua wazi bila kufunga mikanda na hii imechangia maafa mengi barabarani,” alisema Kinyanjui.

“Ni jukumu la kila msafiri kuhakikisha kuwa anafunga mkanda wa usalama kwa maslahi yake mwenyewe na hatupaswi kupuuzilia mbali umuhimu wa mkanda kwa sababu ni kitu ambacho kinaweza kuokoa maisha yako,” akaongeza.

Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa halmashauri yake inafanya kila juhudi ili kuwahamasisha wakenya juu ya umuhimu wa kufunga mikanda ya usalama.

“NTSA inafanya kila iwezalo kuimarisha usalama barabarani lakini hilo litawezekana iwapo wakenya wote watajitolea kuimarisha usalama wao barabarani,” aliongeza.