Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameunga mkono hatua ya Gavana wa Bomet Isaac Ruto kuzindua chama kipya cha kisiasa, atakacho kitumia kutetea kiti chake cha ugavana.

Akihutubu kwenye mkahawa mmoja mjini Nyamira siku ya Jumatatu, Gavana Nyagarama aliwasihi wananchi kujiunga na chama chochote cha kisiasa bila kuruhusu kushurutishwa na wanasiasa kujiunga na vyama wasivyo vipenda.

"Kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa humu nchini ni jambo zuri kwa kuwa hili ni taifa huru na wananchi wana uhuru wa kujiunga na vyama vyovyote vya kisiasa. Wananchi hawapaswi kulazimishwa kujiunga na vyama fulani vya kisiasa na ndio maana nadhani gavana wa Bomet amefanya jambo zuri," alisema Nyagarama.

Gavana Nyagarama aliwahimiza wananchi kutowachagua viongozi wa kisiasa kutokana na vyama vya kisiasa ila tu kupitia kwa utendakazi wao katika jamii.

Alisema kuwa vyama vya kisiasa vilevile vinastahili kukumbatia demokrasia.

"Ningependa kuwahimiza wananchi kuwachagua viongozi kutokana na utendakazi wao na wala sio kutokana na milengo yao ya kisiasa, kwa kuwa wanasiasa hawabadiliki kutokana na miegemeo yao ya kisiasa," alisema Nyagarama.