Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Masaba kaunti ya Nyamira Timothy Bosire amemwomba Gavana John Nyagarama kuagiza maafisa wake waliodaiwa kufuja pesa za umma kuzirudisha ili kutumika kufanya maendeleo tofauti.
Kulingana na mwanasheria huyo, pesa za umma zilizofujwa na kutumika vibaya na serikali ya kaunti ya Nyamira sinastahili kurudishwa ili wananchi wafanyiwe maendeleo walioahidiwa.
Akizungumza siku ya Jumanne katika shule ya upili ya Mokwerero wakati alikuwa anaikabidhi shule hiyo pesa za kujenga madarasa, Bosire alisema ikiwa Nyagarama anahitaji kuungwa mkono na kufanya kazi na wabunge wa kaunti, hiyo sharti pesa zilizofujwa na kutumika vibaya zirudishwe kwanza.
Bosire alikanusha maneno yaliyoandikwa kwa gazeti moja nchini kuwa wabunge wa kaunti ya Nyamira wamekubali kufanya kazi pamoja na gavana Nyagarama, na kusema ni uongo mtupu.
Pia mbunge huyo alisema wabunge wote wa Nyamira hawajawahi kuandaa kikao kuzungumzia makubaliano yoyote au chochote cha maendeleo.
“Sisi wabunge wa Nyamira tunaomba Gavana Nyagarama ajitokeze wazi na kueleza kwa nini pesa zilitumika vibaya na kufujwa na maafisa wengine wa serikali yake,” alisema Bosire.
“Naomba pesa zile zilizovujwa zirudishwe ili zisaidie mwananchi kwa kufanyiwa maendeleo, na baada ya hapo tutakubali kufanya kazi pamoja. Yale yaliandikwa kwa gazeti kuwa tumekubali kushirikiana na Nyagarama ni uongo,” aliongezea.