Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama ameombwa kuupea mradi wa ukarabati barabara kipau mbele kuliko miradi mingine ili kurahisisha sekta ya uchukuzi.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa idadi nyingi ya barabara katika kaunti ya Nyamira zimeharibika pakubwa na kutopika kila wakati inaponyesha na ata ziko na mashimo kila mahali.
Wakizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Kahawa, wadi ya Esise, wakazi wa wadi hiyo walisema changamoto ambazo wanapitia zaidi ni kutopitika kwa barabara, na kumwomba gavana kupea ukarabati wa barabara kipau mbele ili kurahisisha sekta ya uchukuzi katika kaunti hiyo.
John Maisiba, aliyeongoza wakazi wengine, walikiri kuwa kuna baadhi ya barabara ambazo hazijawahi kukarabatiwa na serikali tangu serikali za ugatuzi zianzishwe nchini kwani barabara hizo zinastahili kukarabatiwa na serikali ya kaunti hiyo.
Baadhi ya barabara ambazo walisema hazijawahi karabatiwa miongoni mwao ni ya kutoka kahawa –Manga, Isoge –Riamogambi, na Nyangena–kahawa.
“Tunataka gavana wetu awe katika mstari wa mbele kukarabati barabara za eneo hili na akabidhi mradi wa barabara kipau mbele ikiwa anahitaji uongozi wake kuheshimika,” alisema Maisiba
“Wengine wetu husafirisha maziwa ili kuuza, maindi, maharage lakini barabara hazipitiki, tunaomba atusaidie ili atukarabatie barabara za eneo hili ili kuimarisha sekta ya uchukuzi,” aliongeza.