Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewahimiza wakazi mjini Nyamira kuwa na subira ya kupokea huduma za usambazaji maji bila matatizo kutoka serikali yake kwa ushirikiano na na kampuni ya usambazaji maji. 

Akihutubu siku ya Ijumaa wakati wa kupokea rasmi baadhi ya vifaa vitakavyosaidia kukarabati mabomba na mifereji ya maji, bidhaa zilizopokezwa kampuni ya GWASCO kwa udhamini wa serikali ya taifa la Ujerumani, Gavana Nyagarama alisema kuwa ana hakika vifaa hivyo vya mamillioni ya pesa vitasaidia kurahisisha huduma za maji Nyamira. 

"Baadhi ya pampu za usafirishaji maji ardhini ziliezekwa miaka kadhaa iliyopita na baadhi ya pampu hizo zimezeeka na haziwezi kusafirisha maji, lakini nina hakika kuwa bidhaa ambazo tumezipokea zitasaidia kurekebisha hali ili watu wetu wapate huduma za maji bila ya matatizo," alisema Nyagarama. 

Nyagarama aidha aliwataka wakazi wa mji wa Nyamira kuacha kuharibu pampu za maji kwa nia ya kuiba maji au kuuza pampu hizo, huku akiongeza kusema mradi wa ukarabati pampu utakapotamatika wakazi wa Kebirigo na Rangenyo ndio watakaonufaika pakubwa. 

"Ni himizo langu kwa wakazi wa kaunti hii kuasi tabia ya kuharibu pampu za maji kwa nia ya kuziuza au pia kuiba maji kwa kuwa hali hiyo huathiri pakubwa huduma za usambazaji maji humu Nyamira, ila pindi tu mradi huu utakapotamatika, watu wa Kebirigo na Rangenyo ndio watakaonufaika pakubwa," aliongezea Nyagarama.