Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewahimiza wakazi wa kaunti hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye maeneo makuu ya kaunti zote ndogo ili kupokea mafunzo jinsi yakuthibiti mikasa ya moto kutoka kwa wataalamu wa Marekani.
Akihutubia wanahabari ofisini mwake siku ya Jumatatu, Nyagarama alisema kuwa yafaa wakazi wa kaunti hiyo wapate mafunzo ya jinsi ya kuthibiti mikasa ili kuepuka visa ambavyo kwa muda vimekuwa vikisababibisha uharibifu wa mali.
"Nawahimiza wakazi wa kaunti hii kuchukua fursa ya kuwepo kwa wataalamu hawa hapa Nyamira na kujitokeza kwenye kaunti zote ndogo za kaunti hii kwa minajili ya kupokezwa mafunzo ya jinsi ya kuthibiti mikasa ya moto," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha alisisitiza kuwa serikali yake ina mipango ya kuagiza gari la kuzima moto kwa chini ya miezi mitatu ijayo, huku akiwahimiza wakazi kuwa watulivu serikali inapoweka juhudi za kuhakikisha kuwa mikasa ya aina hiyo inathibitiwa.
"Baadhi ya wakazi wamekuwa wakiishtumu serikali yangu kwa kutonunua gari la kuthibiti mikasa ya moto, ila ningependa kuwaambia kwamba tayari tumeweka mikakati ya kuhakikisha gari hilo limo hapa Nyamira chini ya miezi mitatu ijayo," aliongezea Nyagarama.
Haya yanajiri baada ya mkasa wa moto kuwasababishia hasara kubwa baadhi ya wafanyabiashara katika soko la Kebirigo siku kadhaa zilizopita.