Gavana John Nyagarama amewashtumu wakazi wa eneo la Konate kwa kuzuia magari ya kuzima moto yaliyokuwa yametumwa kuelekea Kebirigo kuthibiti mkasa wa moto ulioteketeza mali ya mamillioni ya pesa wiki jana. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wakazi wa Riomego siku ya Jumapili, Nyagarama alipuuzilia mbali madai kwamba serikali yake ilishindwa kabisa kuthibiti mkasa huo, huku akiwalimbikizia lawama wakazi wa Konate kwa hatua yao ya kuzuia magari hayo. 

"Kutokuwa na magari ya kuzima moto haimaanishi kuwa hatuwezi kuthibiti mikasa ya moto kwa kuwa maafisa wa serikali ya kaunti ya Kisii walithibitisha kuwa baadhi ya wakazi wa Konate walizuia magari mawili ya kuzima moto, hali ambayo ilisababisha sisi kushindwa kuthibiti hali hiyo," alisema Nyagarama. 

Nyagarama aidha aliongeza kwa kuwahimiza maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi na kisha kuwatia mbaroni wale watakaopatikana kuhusika na kitendo hicho kilichosababisha mali ya thamani isiyojulikana kuteketea. 

"Maafisa wa polisi wanafaa kufanya uchunguzi wa haraka na kisha kuwatia nguvuni watu ambao watapatikana kuhusika pakubwa na kitendo hicho katili kwa maana hali hiyo ingethibitiwa mapema isingekuwa watu kuamua kuzuia magari hayo kuelekea Kebirigo," aliongezea Nyagarama.

Akizungumzia swala la serikali ya kaunti yake kununua magari ya kuzima moto, gavana alisema kuwa tayari serikali yake imeweka mikakati ya kununua magari tano yatakayotumwa kwenye kaunti zote ndogo ili kusaidia katika hali ya kuthibiti mikasa hiyo kwa haraka.

"Tayari tumeagiza magari tano ya kuzima moto na yatakuwa yamefika humu Nyamira chini ya miezi miwili ijayo, na kila gari litatumwa kwenye kaunti ndogo kote Nyamira kwa minajili ya kusaidia kuthibiti mikasa," alihoji Nyagarama.