Wakazi wa kaunti ya Nyamira wanaojenga vibanda karibu na sehemu ya barabara zinazo karabatiwa na serikali ya kaunti hiyo wameombwa kubomoa vibanda hivyo ili kurahisisha ukarabati huo.
Akihutubia wanahabari siku ya Ijumaa baada ya ukaguzi wa baadhi ya barabara za mji zinazokarabatiwa, Gavana Nyagarama alisema yafaa wakazi wanaoendesha shughuli zao kando kando ya barabara hizo wahamie sehemu zingine ili kuruhusu ukarabati huo.
"Wale wakazi wanaoendesha shughuli zao kando kando ya barabara hasa Kebirigo-Keroka, Nyamira- Bonyabomite nawaomba waondoke sehemu hizo ili waruhusu wizara ya barabara na kazi za umma kuendesha shughuli zao bila matatizo yeyote kwa maana tunakarabati barabara husika ili kustawisha maendeleo," alisema Nyagarama.
Akizungumzia swala la mabomba ya maji taka kuharibika katika eneo la Gachuba na Kiabonyoru, Nyagarama aliongeza kusema tayari serikali yake imeanza kurekebisha hali hiyo.
"Baadhi ya mabomba ya maji taka na mvua yameharibika kule Gachuba na Kiabonyoru na tayari tumeanzisha mikakati ya kuhakikisha kuwa hali hiyo imerekebishwa mara moja ili kuwaondolea hofu ya wakazi wa maeneo hayo kuambukizwa magonjwa," aliongezea Nyagarama.