Mwenyekiti wa Jomo Kenyatta Foundation (JKF) Walter Nyambati amesema serikali ya kitaifa italeta maendeleo zaidi katika Kaunti ya Nyamira.
Kulingana na Nyambati, aliyekuwa mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba, serikali ya kitaifa imepanga kufaidi wakaazi wa Kaunti ya Nyamira kupitia maendeleo, kwa kuwa ni wajibu wake kutekeleza na kutimiza ahadi za maendeleo.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Nyamira, Nyambati alisema miongoni mwa maendeleo serikali italeta katika kaunti hiyo ni kukarabati barabara na kuinua baadhi ya vyuo vya anuwai, ili kuinua viwango vya masomo katika taasisi za Nyamira.
Miongoni mwa barabara serikali ya kitaifa itakarabati katika kaunti ya Nyamira ni barabara ya Manga-Mote Momwamu, Kemera-Amabuko, Metamaywa-Kebirigo, Chepilat-Chabera na ile ya Nyasiongo-Raitigo.
Wakati huo huo, Nyambati alisema taasisi mbili zitajengwa kwa hali ya kisasa katika eneo bunge la Borabu na katika eneo bunge la Kitutu Masaba.
“Serikali ya kitaifa imepanga kuleta maendeleo mengi zaidi katika kaunti yetu kwani kazi ya serikali ya Jubilee ni kufanya maendeleo. Serikali itatimiza ahadi zote ilizotoa kwa wananchi,” alisema Nyambati.
Aidha, Nyambati aliomba wakaazi wa kaunti ya Nyamira kuungana pamoja na serikali kuu ili kunufaika na maendeleo mengi zaidi.
“Naomba kila mkaazi kushirikiana na serikali ya kitaifa ili kunufaika na miradi ya maenedeleo. Hakuna haja ya kuwa kando na serikali,” alisema Nyambati.