Mbunge wa Mugirango kusini kaunti ya Kisii Manson Nyamweya ameahidi kuimarisha sekta ya elimu katika eneo bunge lake na kuhakikisha watoto wengi wamepata masomo ambayo yatawasaida nyakati zijazo.
Kulingana naye idadi nyingi ya wanafunzi watapata pesa za basari mapema mwaka ujao ikilinganishwa na miaka ya awali ili kujiendeleza kimasomo.
Nyamweya alisema masomo ndio yatasaidia watoto wa kizazi hiki kujiendeleza kimaisha na kusema kuna haja ya watoto hao kupokea elimu ambayo itawanufaisha katika siku zijazo.
Hata hivyo Nyamweya alipongeza walimu wakuu wa shule zote za eneo bunge lake kwa kutumia pesa vizuri kuimarisha ujenzi wa shule na kupongeza kamati za shule pamoja na wazazi kwa ushirikiano huo.
Pia aliahidi kukabidhi shule za upili ya Nyamoya shillingi millioni 2, shule ya upili ya Nyangweta millioni 3 na ile ya Nduru millioni 2.5 ili kutumika kufanya ujenzi.
“Napongeza wazazi, kamati za shule na walimu wakuu katika eneo bunge langu kwa ushirikiano mzuri ambao walikuwa nao kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule mbalimbali umekamilika kwa kutumia pesa vizuri ambazo ni za ustawi maeneo bunge CDF,” alisema Nyamweya.
Nyamweya alipongeza wazazi kwa kuwachukua watoto wao katika shule za eneo bunge hilo kando na hapo awali ambapo wazazi hao walikuwa wanachukua watoto wao katika shule za nje kusoma.
“Nilipoingia katika kiti cha ubunge, shule za eneo bunge langu la Mugirango kusini hazikuwa na wanafunzi lakini nikajaribu nikabadilisha elimu hadi wazazi wakakubali kuleta watoto wao katika shule hizo na ninawapongeza sana,” aliongeza Nyamweya.
Mbunge huyo alikuwa anayaongea hayo siku ya Jumatano na waandishi wa habari mjini Kisii.