Share news tips with us here at Hivisasa

OCPD wa Rongai Joseph Mwamburi amewataka wanandoa na wakaazi katika kaunti ndogo ya Rongai, kutumia afisi za machifu kutatua migogoro baina yao.

Mwamburi alikuwa akizungumza na mwanahabari huyu Alhamisi, kuhusu ongezeko la visa ambapo wananchi wanaripotiwa kujitoa uhai mara kwa mara katika eneo hilo.

“Mwaka huu pekee tumeshuhudia visa visivyopungua sita, vya watu kujitoa uhai ama kuuawa na wengine kwa njia tatanishi. Nahofia watu wasipojihadhari dhidi ya kuchukua sheria mikononi mwao, idadi hiyo itaongezeka mwaka utakapokuwa unatamatika,” alisema Mwamburi.

Siku mbili zilizopita, mzee mmoja kutoka Solai alimshambulia mkewe kwa kisu na kumuua kutokana na mzozo wa kinyumbani, lakini akajisalimisha mikononi mwa polisi wa eneo hilo baada ya umati kutaka kumwadhibu.

Mwishoni mwa mwezi Januari, mshukiwa mwingine alimdunga mwenzake kisu baada ya kuzozania ardhi, na kumuua papo hapo kisha akaenda mafichoni.

“Bado tunamtafuta mshukiwa huyo, na inadaiwa kwamba hapo kabla alikuwa ametekeleza mauaji mengine na akatoroka,” alisisitiza Mwamburi.

Aliwataka raia pia kukoma kuchukua sheria mikononi mwao na badala yake kuwafikisha washukiwa kama hao katika kituo cha polisi.